KILIMO CHA MATIKITI MAJI KIBIASHARA
Habari
ndugu, natumaini unaendelea vyema na juhudi za kuelekea kwenye mafanikio. Nina
uhakika kabisa unatamani kutoka hapo ulipo na kufikia mafanikio, hata kama
tayari umeshafikia kiwango fulani cha mafanikio nina uhakika pia unatamani
kusonga mbele zaidi. Leo ninataka tuanze
kujifunza kuhusu kilimo maarufu kwa sasa hapa nchini, Kilimo cha tikiti maji. Leo
katika mijadala ya fursa za kilimo, kilimo cha tikiti maji hakikosi katika
mijadala hiyo. Hata katika kazi ninazofanya za kutoa ushauri kwa wakulima, wakulima
wengi wamekua wakitamani sana kuingia kwenye kilimo cha tikiti maji na wamekua
wakitamani sana kujifunza kuhusu kilimo hichi. Umaarufu na Kupendwa kwa kilimo
hichi kunasababishwa na mambo mawili makubwa: Kwanza ni kilimo cha muda mfupi
(miezi 2 hadi 3) kiasi kwamba mkulima anaweza kulima hadi mara nne kwa Mwaka,
Pili ni Kipato kinachopatikana, pamoja na kwamba kuna changamoto zake, lakini
ukiweza kufuata kanuni na kulilenga soko vizuri (timing ya soko) unaweza kupata
kicheko cha pesa kizuri sana. Wapo wanatengeneza faida zaidi ya milioni 5 kwa
ekari nawapo wanaopata hasara. Sasa blog yako ya Kilimo biashara
(www.kilimobiashara.net) inaanza kutoa mafunzo ya kilimo cha tikiti, tunaamini
ukifanyia kazi mafunzo haya kupata faida kubwa kwenye zao hili itakua ni jambo
la kawaida sana kwako. Fuatana nasi katika makala hizi za kilimo cha tikiti,
hatukuelekezi tu jinsi ya kufanya, bali tunakufundisha pia ni kwanini kifanyike
hivyo. Karibu sana.
Utangulizi
Tikiti
maji ni zao linalolimwa kibiashara.hufahamika kama Watermelon, na kwa jina la
kibotania (Botanical name) hujulikana kama Citrullus
lanatus. Ni moja ya mazao yanayotoka kwenye familia ya mimea ya
Cucurbitaceae, mazao mengine ynayotoka family hiyo mojana tikiti maji, ni matango
(Cucumber), maboga (pumpkin), musk melon, squash n.k. Inaaminika kwamba asili
ya tikiti maji ni huko jangwa la Kalari ambako lilikua linapendwa sana kwa
sababu lilitumika kupooza koo au kukata kiu kwa watu wanaoishi karibu na Jangwa
la Kalahari hii ni kwasababu tikiti maji ni tunda lenye maji mengi. Inakadiriwa
zaidi ya asilimia 90 ya runda la tikiti ni maji, ndio maana huitwa tikiti maji.
Hata hapa Tanzania Tikiti maji soko lake zuri ni kipindi cha joto ambako walaji
wengi hutumia kwa ajili ya kukata kiu kutokana na joto. Wauzaji wa matikiti
katika masoko mabalimbali wanasema biashara ya tikiti ni nzuri sana wakati wa
kiangazi/joto na wakati wa baridi biashara hiyo inadorora. Taarifa kama hizo ni nzuri sana kwa mkulima
mjasiriamali anayelenga uhitaji wa soko.
MAANDALIZI YA SHAMBA:
Shamba
la kupanda matikiti maji linapaswa liandaliwe vizuri, udongo ulainike vizuri
usiwe na mabonge ya udongo kwa maana mbegu za tikiti zinapdwa moja kwa moja
shambani (direct seeding) na mbegu hizo
zina umbo dogo, hivyo zinahitaji udongo uliolainika vizuri ili kuweza kuota.
Shamba linapaswa kua sehemu ambayo hakuna miti, maana kivuli cha miti kinaweza
kusababisha matikiti yasitoe matunda.
Vifuatavyo
ni Vigezo vya kuzingatia wakati wa kutafuta shamba/eneo la kupanda matikiti
maji.
1.
Aina ya Udongo
Tikiti maji linaweza kulimwa katika aina
nyingi za Udongo, lakini yanafanya vizuri zaidi kwenye udongo kichanga (fine
sand), tifutifu na tifutifu kichanga. Aina ya udongo itaadhiri uzalishaji wa
tikiti kutegemeana na hali ya hewa. Kwa mfano unapolima tikiti kwenye udongo wa
mfinyazi wakati kuna mvua nyingi, mimea
ya matikiti haitaweza kustawi, kwa sababu udongo wa mfinyazi utatuamisha maji
kwasababu ya mvua na hivyo mimea itakufa. Vilevile unapootesha matikiti kwenye
udongo wa kichanga, halafu pawe hakuna maji ya kutosha mimea itakufa kwa kukosa
maji. Pia kumbuka udongo wa kichanga unapoteza maji kwa haraka, hivyo unapolima
kwenye udongo wa aina hiyo hakikisha una maji ya kutosha na umwagiliaji uwe wa
mara kwa mara.
2.
Utoaji wa maji shambani (Drainage).
Kigezo kingine ambacho mkulima anapaswa
kuzingatia wakati wa kutafuta eneo la kupanda matikiti ni Udongo wenye uwezo wa
kutoa maji, yaani udongo usiotuamisha maji. Unaweza kutengeneza mifereji
itakayoasaidia kuondoa maji yanayozidi shambani.
3.
Mteremko wa Ardhi (Topography)
Ni ile hali shamba linapokua limeinuka upande
mmoja na upande mwingine kuna mteremko au unaweza kuiita slope. Shamba lenye
mteremko au slope ni rahisi sana kukumbwa na mmomonyoko wa udongo ambao utaharibu
mimea yako. Hakikisha unapoachagua shamba, basi unaepuka maeneo ya mtindo huo.
4. Mwanga wa jua (Sunshine).
Katika
upandaji wa zao lolote mwanga wa jua ni muhimu sana kwasababu husaidia kwenye
utengenezaji wa chakula cha mmea (Photosynthesis). Kwa upande wa matikiti,
mwanga wa jua una athari kubwa sana kwenye mazao, aidha kupungua au kuongezeka.
Mmea wa Tikiti unahitaji angalau masaa 6
ya mwanga wa jua. Hii inasaidia sana katika utengenezaji wa sukari kwenye
tikiti. Pia mwanga wa jua husaidia ukuaji wenye afya wa mmea wa tikiti. Hivyo
kwa ukuaji mzuri, unapochagua eneo la kulima tikiti chagua eneo ambalo Mimea
itapata mwanga wa jua wa moja kwa moja (direct sunlight) kwa angalau masaa 6
hadi 8 kwa siku. Hii ikimaanisha kwamba eneo liwe mbali na majenngo au miti
mikubwa inayoweza kuleta kivuli kwenye shamba.
Madhara ya
Kukosa Mwanga wa Kutosha
·
Matikiti yaliyopo
eneo lenye mawingu ya mara kwa mara au eneo mbalo halipati mwanga wa jua wa
kutosha, huzaa matunda yenye ladha mbaya.
·
Mimea ikikosa
mwanga, hunyauka na kufa.
·
Uchavushaji
(pollination) kwenye Mimea ya Matikiti hufanywa na wadudu kama nyuki, Shughuli
za nyuki zinapungua wakati wa baridi au wakati wa mvua kwa sababu vipindi hivyo
hakuna mwanga wa jua wakutosha. Hii ina maana kwamba hata eneo lenye kivuli sio
rafiki kwa shughuli za uchavushaji
·
Matikiti
yanahitaji joto ili kuzalisha matunda matamu. Hii ikimaanisha kama eneo litakua
lina kivuli halitakua na joto hivyo matunda yatakosa sukari
5. Maji
Upatikanaji wa maji katika eneo la kuzalishia
matikiti ni kigezo kingine muhimu cha kuzingatia wakati wa kuchagua eneo. Ili
kufanya kilimo chenye uhakika, jitahidi eneo lako liwe karibu na chanzo cha
maji cha uhakika, kwa ajili yakufanya umwagiliaji.
6. Kufikika.
Eneo liwe sehemu kunakofikika hususani kwa miundombinu ya barabara. Eneo liwe mahali
ambapo gari kubwa inaweza kufika, ili kusaidia usafirishaji wakati wa kuvuna.
AINA ZA
MBEGU NA UCHAGUZI WA MBEGU NZURI
Uchaguzi wa aina ya mbegu (variety) ni kitu
cha msingi sana katika kilimo cha tikiti ambapo shughuli zote zinajengwa kwenye
msingi huo. Hii kimaanisha kama ukikosea kuchagua aina ya mbegu nzuri hata
ukijitahidi mbinu nyingine, hazitakua na tija.
Kuchagua mbegu nzuri na zenye ubora sio kazi nyepesi, ni ngumu kweli
kweli, kwa bahati mbaya wakulima wengi hukimbilia zile mbegu maarufu ambazo
zinatangazwa zaidi, ambapo mara nyingi wanapokwenda kwenye uhalisia kwa kulima
mbegu hizo hukumbana na hali tofauti na waliyoisikia kwenye matangazo.
Vigezo vya
muhumu kuzingatia wakati wa Kuchagua Aina ya Mbegu:
Kabala mkulima hajafanya maamuzi ya mbegu ipi
alime, ni vyema akazingatia vigezo vifuatavyo:
Ni aina ipi
ambayo ina soko? Kama unalima
kibiashara, hichi ni kigezo cha kwanza kuzingatia, tambua kwanza soko
unalolenga linapendelea aina ipi ya matikiti. Kwa mfano kwa kanda ya ziwa,
matikiti yenye mistari ya Zebra, hayana mpenyo kwenye soko la kanda ya ziwa,
walaji wengi bado wanapendelea yale matikiti ya kijani au wengine wanayaita
meusi, yasiyokua na mistari au mabakamabaka. Sasa kwa kusikia maeneo mengine
kama Arusha na kwingine kwamba watu
wanalima matikiti ya mistari ya zebra na Wewe uko kanda ya ziwa , halafu ukaingia kulima hayo ya Zebra wakati soko
lako unalolenga ni Mwanza, lazima wakati wa kuuza utalalamika hakuna soko.
Hivyo ni muhimu kufahamu soko lako kwanza, jua linahitaji aina ipi
kisha ndio ufanye uamuzi wa kulima aina ipi.
Uwezo wa
kumudu au kukubali mazingira utakayolimia (adaptability). Sio aina zote za matikiti zinakubali kila
aina ya mazingira, kuna maeneo ambayo
aina fulani inakubali, na ila aina nyingine ikagoma. Hivyo fahamu uwezo wa aina
hiyo ya tikiti kuota kwenye mazingira yako. Kama kuna majirani wanaolima matikiti au watu wa maeneo ya
karibu na mazingira yako wanalima tikiti, unaweza kufanya utafiti wako kwa
kujua ni aina ipi inafanya vizuri kwa hao majirani zako.
Angalia
gharama za kuhudumia/matunzo.
Kuna aina za tikiti zinahitaji matunzo ya gharama kubwa kama vile mbolea za
kutosha, madawa n.k. Hivyo ni muhimu kujua gharama zake kabla hujanunua, ili
kama uwezo wako hautamudu, uchague aina nyingine, ili usije pata hasara kwa
kuchukua aina yenye kuhitaji matunzo makubwa ukashindwa kuyahudumia
UPANDAJI
Katika upandaji wa tikikiti zipo aina nyingi
za upandaji, ila kwa hapa tutagusia aina mbili ambazo zina matokeo mazuri:
Upandaji wa
Mstari mmoja (Single row system). Hapa
tuta linakua na mstari mmoja tu wa tikiti. Nafasi ya mstari hadi mstari ni mita
2 au mita mbili na nusu (2 – 2.5m). Nafasi ya mche hadi mche ni sentimita 60.
Upandaji wa
Mistari miwili (double row system).
Hapa tuta linakua na mistari miwili ya tikiti. Nafasi ya mstari hadi mstari ni
mita tatu na nusu hadi mita nne (3.5 – 4.0m). Nafasi ya mche hadi mche ni
sentimita sitini (60cm).
Kwenye shimo moja zinapandwa mbegu mbili, kama
zikiota zote mbili, basi moja unaing’oa na kuhamishia kwingine ambako kunaweza
kua ni sehemu mpya kabisa au ni hapohapo shambani, kwenye shimo ambalo
hazijatoata au ziliota zikafa.
UWEKAJI WA
MBOLEA
Mbolea ya Samadi: Weka shamba lako mbolea ya
samadi iliyokauka vizuri. Kiasi kinachotosha ni tani 5 had 8 kwa ekari moja.
Mbolea za kupandia: Mbolea ya kupandia unaweza
kutumia DAP, Minjingu au mbolea yeyote yenye kirutubisho kikubwa cha
Phosphorous. Mbolea ya Kupandia inawekwa wakati wa kupanda, kwenye shimo la
kupandia, unatanguliza mbolea ya kupandia wastani wa gramu 5, kisha unafunika
na udongo kidogo kisha ndio mbegu ya tikiti inafuata. Lengo hapa ni mbegu
isigusane na mbolea ya kupandia.
Mbolea za Kukuzia: Mbolea za kukuzia ni zinazotumika
sana kwenye kilimo cha tikiti ni kama NPK, na CAN.
Mbolea za Majani (foliar fertilizers). Hizi ni
mbolea zinazowekwa kwenye majani kama
unavyopulizia dawa (spraying). Mbolea hizi hua ni zile zenye vile virutubisho
vinavyohitajika kwa kiwango kidogo (micronutrients). Unapiga mara matikti
yanapoota, kisha unapiga tena wakati wa utoaji wa maua, halafu unamalizia na
wakati wa utengenezji wa matunda.
MAGUGU NA
PALIZI
Magugu yana madhara kwa zao lolote, ila yana
madhara makubwa zaidi kwa zao la tikiti maji. Lakini ni muhimu kufahamu kwamba
Udhibiti wa magugu au palizi kwenye matikiti kunahitaji umakini sana kwa maana
tikiti hazihitaji kubugudhiwa au kuguswaguswa/kutingishwatingishwa maana
husababisha mmea mzima kupata stress kitu ambacho kitaathiri mpangilio wa
uzalishaji. Palizi pia inaweza kuharibu maua au matunda yale madogo yaliyoanza
kutengenezwa.
ATHARI ZA
MAGUGU KWENYE UZALISHAJI WA MATIKITI MAJI
Magugu yanashindania virutubisho na mazao
(compete with plant for nutrients). Na magugu yana uwezo mkubwa wa kutumia
virutubisho kuliko mazao, ndio maana magugu yanakua kwa haraka kuliko mazao
yaliyopo shambani. Hii hupelekea uzalishaji wa tikiti kupungua.
Magugu yanashindania maji na mazao ya tikiti,
na kupelekea tikiti kukauka. Kama ilivyo kwa virutubisho hivyohivyo magugu yana
uwezo wa kutumia maji haraka kuliko mazao.
Magugu yanapunguza utoaji wa maua kwenye
tikiti kutokana na kupungua kwa mwanga wa jua. Magugu husababisha kivuli kwa
matikiti hivyo kukosa mwanga wa kutosha ambao husaidia mimea kutoa maua.
Magugu pia yanapunguza utoaji wa matunda
kwenye mmea. Maua yakiwa machache hasa maua ya kike ina maana matunda
yatakayotengnezwa yatakua machache zaidi.
Magugu yanazuia shughuli ya uchavushaji
(pollination) shaghuli ambayo ni muhimu sana kwenye kilimo cha matikiti. Hii
ina maana wadudu wanaofanya ushavushaji kama Nyuki, watakimbilia kwenye maua ya
magugu na kuacha kushughulika na maua yamatikiti.
Magugu pia yanavutia wadudu na magonjwa kwenye
mazao
UTHIBITI WA MAGUGU
Mpaka wa sasa hakuna madawa chaguzi (selective
herbicides) ya kufanya palizi kwenye tikiti.
Madawa chaguzi, ni yale madawa ambayo unapiga shambani alafu yanaua
magugu lakini hayana madhara kwa mazao. Mfano dawa yenye kiambato (active
ingredient) cha Oxyfluorfen ya kupiga kwenye vitunguu, inapopigwa kwenye
shamba la vitunguu, inaangamiza magugu lakini vitunguu vinabaki salama. Kwa
upande wa zao la tikiti bado hakuna dawa za namna hiyo.
Hivyo magugu kwenye tikiti yanahitahitji
kufanyiwa palizi kwa mkono au jembe wakati mimea ikiwa midogo. Epuka kufanya
palizi wakati tikiti limeshaanza kutoa maua.
Kama umefanya palizi mapema na bado kipindi
cha utoaji maua pakawa na mgugu basi subiri kidogo, kipindi cha utoaji maua
kikiisha tu, basi ng’oa hayo magugu kwa mkono, huku ukiepuka kugusagusa mimea
ya tikiti.
Uwekaji wa
Matandazo (Mulching)
Njianyingine ya kudhibiti magugu ni njia ya
kuweka matandazo (mulching). Kuna ana mbili za matandazo, ambayo ni matandazo
ya Asili (orgnic Mulch) na Matandazo yasiyo ya asili (inorganic mulch).
Uwekaji wa
matandazo ya asili (Organic mulching)
Njia hii inatumia nyasi/majani yaliyokauka, vumbi
la miti (saw dust) au wengine wanayaita maranda. Maranda (Saw dust) ni yale
masalia yatokanayo na upasuaji wa miti au mbao. Nyasi au maranda hayo
yanatandazwa shambani. Ukipata maranda ni nzuri zaidi, maana baadaye yataoza
haraka shambani na kuwa mbolea.
Uwekaji wa
matandazo yasiyo ya asili (Inorganic mulching)
Njia hii ni utmiaji wa matandazo ya karatasi
za plastic (plastic mulching) kudhibti magugu. Hapa karasi nyeusi (black
polythene) ndiyo inatumika maana hairuhusu magugu kuota. Pia inasaidia kuhifadhi
unyevunyevu kwenye udongo kwa maana zinapunguza upoteaji wa maji (evaporation).
Faida yake nyingine ya njia hii ni kwamba inadumu muda mrefu zaidi ya matandazo
ya asili. Matandazo haya (karatasi ya plastic)
yanaweza kutumika hata kwa misimu zaidi ya mine bila kubadilisha.
UMWAGILIAJI
WA MATIKITI
Matikiti maji aslimia 90 yake ni maji, hivyo
yanahitaji maji ili kukua. Mizizi ya mmea wa tikiti huenda chini sana kutafuta
maji kwa ajili ya kusaidia matunda yenye njaa ya maji. Mwagilia mimea maji ya
kutosha, ili angalau maji yaingie inchi 6 kwenda chini. Hii itafaa zaidi kama
unatumia mifumo ya umwagiliaji wa matone (drip irrigation system). Matikiti
maji yanahitaji maji kipindi chote cha ukuaji, ila kipindi cha muhimu zaidi ni
wakati yanapotengeneza matunda na wakati wa ukuaji wa matunda. Kama maji
yasipotosha kipindi hichi, tunda halitaweza kukua kufikia uwezo wake wa mwisho
(full potential), na inaweza kusababisha tunda kudumaa au kusababisha
kudondoka. Kipindi hichi ni cha kuhakikisha mimea inapata maji kwa gharama
yoyote.
Maji pia yanaweza kuharibu ubora wa matikiti
endapo yatawekwa wakati ambao sio na kwa kiwango kisicho sahihi. Ikiwa na maana
kwamba kipindi maji yanapohitajikwa kwa wingi, basi yawekwe kwa wingi, kipindi
yanapohitajika kwa uchache basi yawekwe kwa uchache.
Maji ya umwagiliaji yanapaswa kudhibitiwa wiki
mbili baada ya kutengeneza matunda, ili sukari iweze kutengenezwa vizuri. Usipodhibti
maji kipindi hichi, maji yakizidi hupelekea matunda kukosa sukari na hivyo
kukosa ladha, na kukosa ladha ni kupunguza ubora tikiti. Epuka uwekaji wa maji
kipindi cha uvunaji kwa maana matunda yatapasuka na kusababisha kuoza.
UVUNAJI WA
MATIKITI MAJI:
Hii ndiyo shughuli pkee katika uzalishaji wa
matikiti isiyohitaji fedha zaidi bali ujuzi. Wakati huu kila mkulima ana shauku
ya kuonja bidhaa yake ili kuona ina ladha gani. Tatizo sasa linakuja pale
ukiambiwa utenganishe matikiti yaliyoiva na yale ambayo hayajaiva. Kama huna
ujuzi utajikuta unaharibu matikiti mengi kwa kuyaonja ili kujua kama yameiva.
Jinsi ya
Kutambua matikiti yaliyoiva (Baadhi ya dalili za Matunda yaliyoiva):
Kutambua matikiti yaliyoiva ni kazi rahisi
sana, lakini kama huna maarifa utajikuta unavuna matunda ambayo hayajaiva kitu
ambacho kitapunguza ubora wa matunda yako. Tikiti lililoiva linatambuliwa kama
ifuatavyo:
1. Tazama tumbo lake. Tumbo la tikiti ni ile
sehemu ya upande wa chini wa titkiti iliyogusana na ardhi. Kwa tikiti lililoiva
sehemu hii inayogusana na ardhi hua ya njano na sio nyeupe kama inavyokua
kwenye matikiti ambayo hayajaiva.
2. Lipige kwa kidole au mkono. Tumia kidole chako
kwa upande wa kucha au kiganja chako, kupiga tunda la tikiti pale katikati ya
tunda kwa ubavuni. Tunda lililoiva litakua na sauti ya kama kuna uwazi kwa
ndani unapoligonga. Au sauti ya ngoma.
Tikiti
maji hutumia siku 60 hadi 120 toka kupanda hadi kukomaa, inaegemea zaidi na
aina ya tikiti. Mfano zipo aina nyingine zinatotumia siku 60 hadi 80 kama sugar
baby, MSHINDI F1, ANDAMAN F1, ADITI F1, zinatotumia siku 80 hadi 90 kama Sukari
F1, Zebra F1, ANDAMAN F1, na zipo zile zinazochukua siku 100 hadi 120 kama Pata
Negra F1. Mavuno ya tikiti hutegemea sana aina ya tikiti na matunzo. Unaweza
kupanda aina zenye mavuno makubwa lakini matunzo yakawa duni, usitegemee kupata
mavuno makubwa. Aina nyingi za chotara (Hybrid) zinauzao wa tani 15 hadi 25 kwa
ekari (15 – 25 tones/acre)
Stori ya Mkulima aliyetengeneza
million 30:
Mwezi
huu mwanzoni, nilikua kwenye shughuli za kuwatembelea baadhi ya wakulima katika
wilaya ya Sengerema, nilipata wasaa wakufika kwenye mashamba ya baadhi ya
wakulima. Nikiwa kwenye shambala la mkulima mmoja katika kata ya Kasenyi, hapo
shambani kulikua na wakulima kama 3 wengine, katika mazungumzo, ikaibuka stori
ya kilimo cha matikiti kwamba ni dili sana kwa siku za leo. Kuuliza kwanini
wakasema kuna mkulima mmoja hapo kijijini amekua ndio stori ya mjini kwa huko
kwao, maana msimu uliopita alipata Milioni 30, (30,000,000) kwenye Kilimo cha
tikiti. Nilipata hamasa ya kutaka kufahamu zaidi kuhusu huyo mkulima, na namna
alivyoweza kupata kicheko kikubwa hivyo. Katika kuendelea kudadisi kwa kuuliza
maswali, nikagundua kwamba mkulima huyo Alilima zaidi ya ekari 10, yaani hiyo
milioni 30 aliipata kwenye hizo ekari zaidi ya 10. Kufanya mahesabu sawasawa,
nikagundua kwamba kila ekari alipata milioni 2 na laki kadhaa tu. Kwa mkulima
ambaye hayuko kimahesabu akiisikia hiyo milioni 30 anaweza kuona kama ni faida
kubwa sana, lakini sio kubwa kivile kama walivyokua wanamwaga sifa. Kwa idadi
ya ekari alizolima mkulima huyu, alipaswa akianguka sana basi ni milioni 40.
Nilichogundua ni kwamba wakulima wengi wao wanaangalia zaidi Mapato Ghafi
(Gross income) yaani yale mapato anyaoyapata baada ya kuuza mazao yake, bila
hata ya kutoa gharama alizotumia kuzalishia wakidhani ndio faida. Moja ya ujuzi au uwezo
anaopaswa kua nao mjasriamali yeyote ni Uwezo wa kufanya mambo kimahesabu. Kabla
ya kuanza kilimo fahamu gharama unazohitaji kuwekeza kwenye hicho kilimo, halafu weka kumbumbukumbu ya gharama halisi
unazotumia, ili badaye uweze kufahmu umepata faida kubwa, ndogo au umepata
hasara.
Tunazo
Huduma ambazo zinaweza Kukupa faida kubwa kwenye kilimo cha tikiti kuliko huyu
mlima wa million 30.
Huduma
ya Kwanza: Uchambuzi wa Gharama na Faida (Cost benefit Analysis - CBA) wa Zao lolote utakalotaka kulima Kibiashara.
Kwanini
CBA? Baadhi ya Manufaa ya kuanza na CBA ni:
CBA
itakusaidia kujua Rasilimali na gharama zinazohitajika kwenye uwekezaji wa
kilimo unachotaka kufanya. Hii itakusaidia kufanya maamuzi ya kuendelea na wazo
la kulima zao hilo au itakubidi ufanye zao lingine.
CBA
itakusaidia kujua makadirio ya mapato faida utakayopata. Hakuna mtu anayependa
kufanya kitu bila kujua manufaa ya kile anachokifanya. Hivyo CBA itakupa picha
ya kile utakachokipata.
CBA
itakusaidia kujua mgawanyiko wa gharama zinazohitajika. Mfano kama kilimo cha
tikiti kinahitaji mtaji wa milioni 2. Haina maana kwamba lazima uwe na hizo
milioni mbili ndio uanze kilimo cha tikiti. Inaweza kua inahitajika laki 5,
halafu baada ya mwezi ikahitajika milioni moja, halafu mwishowe ikahitajika
laki 5. Sasa bila kujua mgawanyiko huo unaweza kudhani ni ngumu kufanya kilimo
cha tikiti kwasababu ya mtaji mkubwa unaohitajika, kumbe unaweza kuanza na
kiasi fulani. CBA itakupa picha kamili kwenye hilo.
- Huduma hii pia inaambatana na ushauri wa mbegu nzuri kulingana na soko unalolilenga na ukuaji wake kwenye eneo unalotaka kulima. Pia namna ya kuipata mbegu Halisi (maana moja ya changamoto kwenye zao la tikiti ni kwamba baadhi ya mbegu ni feki, unaweza kununua mbegu ghali na mwishowe kumbe umechukua feki)
Huduma
hii inapatikana kwa gharama ndogo ya 20,000/= (Elfu Ishirini tu).
Huduma
ya Pili: Master Plan. Huu ni Muongozo au Mpango kazi wa Kilimo cha zao la
Tikiti.
Mpangilio
huu unakuonyesha shughuli zote za Shambani na muda wake wa kufanyika. Hii
itawasaidia sana wale ambao wanataka kufanya kilimo lakini hawajui kipi kianze
na kipi kifuate. Pia utawasaidia kuongeza faida wale ambao wamewahi kulima
kilimo cha tikiti lakini hawakupata faida waliyotegemea. Muongozo huu
utakuonyesha aina ya mbolea na kiasi kinachohitajika, aina za madawa ya
magonjwa na wadudu na kiasi gani cha uchanganyaji wa dawa hizo,
Umwagiliaji, na mambo mengine mengi.
Gharama
ya kutengnenezewa Mungozo (Master Plan) ni 20,000/= (Elfu Ishirini tu).
Kwa
watakaohitaji Huduma zote mbili watafanyiwa kwa 30,000/= (Elfu thelathini tu)
Kwa
swali lolote kuhusu kilimo au ushauri, au kupata huduma zetu Waweza kuwasiliana
nasi kwa Namba 0763 071007 au kupitia email yetu: ushauri@kilimobiashara.net
Asante
na Karibu sana. Tukutane wakati mwingine.
Daudi
Mwakalinga
www.kilimobiashara.net
Kama ulikua hujasma makala ya Kilimo cha Vitunguu basi bonyeza hapa: Lima Vitunguu Kijanja.
Chanzo:Kilimobiashara blog
Post a Comment