Umuhimu Wa Kuwa Makini Katika Nyanja Mbalimbali Za Maisha
Habari za wakati huu ndugu msomaji wa makala za mtandao huu, ni matumaini yangu kuwa hu mzima na unaendelea vizuri katika kuhakikisha kuwa unapambana ili kujiletea mafanikio. karibu tena Leo tujifunze kwa pamoja juu ya umuhimu wa kuwa makini katika nyanja mbalimbali za kimaisha.
Leo hii kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kumekuwa na mabadiliko pia katika nyanja mbalimbali za maisha mfano kumekuwa na mabadiliko katika njia za upashanaji habari, kilimo,biashara,upataji elimu n.k. Leo hii anaweza akatokea mtu na kukushauri juu ya jambo fulani anaweza kuwa ni mtu muhimu sana maishani mwako, lakini hili halitoshi kukufanya wewe ukubaliane nae moja kwa moja juu ya yale anayokuambia hata pasipo kutilia umakini wowote ule ushauri wake. Ni muhimu kupata ushauri toka sehemu mbalimbali tena ni muhimu sana sana lakini sio jambo la busara kuukubali kila ushauri pasipo umakini katika kuupembua ushauri huo. Hivyo kwa kila ushauri unaopewa hakikisha unafanya upembuzi wa makini ili ujiridhishe ndipo uufuate ushauri huo, kuwa makini katika ushauri unaopewa.
Leo hii ukipita pale au kule utasikia watu wanasema kilimo kinalipa, kilimo kinalipa nikuulize swali rahisi, pindi. usikiapo hivyo huwa unamakinika vipi na ukweli wa kauli hizi au na wewe huwa unakurupuka na kujiingiza katika kilimo husika pasipo kufanya uchunguzi au kumakinika na taarifa hizi.
Labda niseme naposema kumakinika au umakini unahitajika narejelea nini?, hapa ninalo rejelea ni kuepuka ile Hali ya haraka haraka au kiherehere katika kila unalolisikia badala yake, unatakiwa kuwa mtulivu, fanya tathimini, chunguza, tafuta ukweli na ufikiri mambo muhimu juu ya lile uliloliona au kulisikia.
Leo hii kuna biashara mbalimbali zimezuka hasa hizi biashara za mtandao biashara hizi sisemi kuwa ni mbaya lakini nyingine zina uwalakini ndani yake, naomba unisikilize kwa makini yaani umakinike ili unielewe kwanini natilia mashaka baadhi ya biashara za mtandao, baadhi ya biashara hizi zimejaa uhamasishwaji juu ya faida na unapigiwa hesabu za haraka haraka na kuoneshwa jinsi utakavyo kuwa tajiri. Hivi Leo hii wewe unaamini kuwa kitendo cha wewe kumuunga mtu katika sehemu fulani unapata hela na yule akimuunga unaendelea kupata sasa hiyo ni biashara au mchezo wa kuunganishana kwenye makundi?. Unapopewa wazo la biashara fikiri juu ya mazingira yako, fikiri juu ya wanaokuzunguka hivi wakisema umuunganishe mtu angalia ni mtu gani wa karibu nawe anaweza kujiunga kati ya kumi ukipata mmoja jua kuna shida hapo. Kumbuka sikatazi wala kupinga biashara za mtandao bali nasisitiza umakini katika maamuzi ya kujiunga na biashara hizi hasa ukizingatia maana ya biashara ambayo kwa mujibu wa webster dictionary wanasema biashara ni shughuli ya kutengeneza,kuuza au kununua bidhaa au huduma kwa kutumia pesa. Zingatia hiyo maana ya biashara ili pindi unapopata au wazo la biashara uzingatie hili na kujiridhisha kuwa hiyo ni biashara au mchezo wa kuunganishana.
Unahitaji umakini katika kuchagua ni yupi awe mke au mume wako, na sio kuongozwa na mizuka au tamaa ya Mali,mwonekano, kabila,familia anayotokea na mengineyo. Kumbuka ukikosea kuchagua mke au mume dunia hii utaiona ni uwanja wa Fujo.
Unahitaji umakini katika kuchagua nani awe rafiki yako na yupi asiwe, nani awe mshauri wako na yupi asiwe n.k. unahitaji kuwa makini juu ya ni kipi usome Ili kujiimarisha na kipi usisome.
unahitaji kuwa makini katika malezi ya wanao na sio kujitia uko bize na biashara au kazi za ofisini, huku ukimwachia Dada wa kazi (house girl) jukumu la kulea watoto wako wakati wewe ndiye mzazi.

Post a Comment