Aina Mbili (2) Za Mabadiliko Na Namna Ya Kuyatumia Katika Kupangilia Maisha Yetu Ya Sasa Na Baadae.
Habari rafiki, ni
matumaini yangu kuwa hu mzima na unaendelea vyema katika kupambana ili
kujiletea mafanikio, naomba nikupongeze sana kwa uamuzi huo uliouchukua maana
ni uamuzi wa msingi sana na wenye tija. Karibu tujifunze kwa pamoja leo aina
mbili za mabadiliko na jinsi ya kuyatumia mabadiliko haya katika kupanga maisha
yetu ya sasa na baadae.
Katika maisha tunayoishi
kuna mabadiliko ya aina mbalimbali ndio maana ulivyo leo hii sio kama
ulivyokuwa miaka mitano huko nyuma wala sio kama utakavyokuwa miaka kumi au
mitano ijayo mbele. Lakini yote hii itategemeana na ni kwa jinsi gani umeweza
kupambana katika kuhakikisha kuwa unayatumia mabadiliko katika maisha yako.
Aina ya kwanza ya
mabadiliko ni mabadiliko yaliyopo katika mzunguko yaani
mabadiliko haya huwa ni ya vitu ambavyo huwa vinajirudia na marudio yake
yamefanya iwe mazoea kwetu. Mfano wa mabadiliko haya ni kama vile kupanda na
kuvuna, kuzaliwa na kufa, majira ya mwaka, soko la hisa n.k. Ukitazama mifano
hii mfano, mfano wa soko la hisa utakuja gundua kuwa kuna wakati bei ya hisa
huwa chini na kuna wakati huwa juu, hivyo basi kwa aina hii unaweza kujiwekea
malengo ya wakati fulani. Mfano ukanunua hisa leo ukakaa nazo mpaka utakapo
kuja kuona bei ni nzuri na yenye tija ndipo unaziuza lakini kutokana na
mzunguko wa pesa unaweza kutabiri soko la hisa litakuwaje na maisha ya
wafanyabiashara wa hisa yatakuwaje.
Kupitia majira ya mwaka
unaweza kutambua kuwa kipindi hiki ni cha kufanya shughuli fulani na kipindi
hiki sio cha shughuli fulani hiyo ni katika kutazama maisha ya sasa, lakini
katika kuyatazama maisha ya baadae unaweza kuangalia mabadiliko ya majira na
ukatabiri kitu na hatimaye ukachukua hatua. Mfano mabadiliko ya majira katika
baadhi ya sehemu yanaweza kuashiria kuwa kuna baadhi ya sehemu huko mbeleni
zitakuwa jangwa n.k.
Aina ya pili ya
mabadiliko ni mabadiliko ya moja kwa
moja, aina hii ya mabadiliko ni mabadiliko ambayo hayapo katika mzunguko
yaani yakitokea hayarudi tena sio kama
kuvuna na kupanda ambako hujirudia hapana, mabadiliko haya huwa kama kuchomwa
kwa karatasi yaani ikiungua yanakuwa majivu na majivu hayawezi kurudi kua
karatasi tena. Hapa ndipo nataka nipasisitizie kwa makini sana. kutokana na
sababu mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza hapa duniani zimekuwa zikileta
mabadiliko ya moja kwa moja ambayo hayawezi kujirudia tena. Mfano katika sehemu
ambazo kwa sasa zinajengwa barabara za lami kuna kuwa na fursa mbalimbali, mfano
watu kuajiriwa katika vitengo mbalimbali, kuna wanaoweza pata manufaa kutokana
na kupangisha nyumba kwa wafanyakazi, wengine wakapata fursa ya kuuza chakula
n.k. haya ni mabadiliko ya moja kwa moja.
Kwanini ni ya moja kwa
moja kwa sababu fursa hiyo haiwezi kujirudia tena, kwa nchi yetu hii lami
ikiwekwa ndo ishatoka hakuna kuweka lami mara nyingine yanabaki ni marekebisho
madogo madogo tu. Hivyo leo hii jua kucheza na mabadiliko haya ili uweze kuja
kuishi vizuri baadae maana ukishindwa utakuja kupata shida baadae.

Post a Comment