Hii Ndio Sababu Ya Wengi Kukosa Ujuzi Katika Uongozi Iwe Kwao Binafsi Au Kwa Wengine.
Uongozi ni sifa ambayo kila mtu angependa
kuwa nayo katika maisha yake, lakini ukweli ni kwamba watu wengi wameamua kuwa wafuasi badala ya
kuwa viongozi. Mpaka hapo unaweza ukawa unajiuliza, inawezekana vipi mtu
akaamua kuwa mfuasi? Tambua kwamba chochote kile unachokifanya au kutokufanya
katika maisha huwa kinatokana na maamuzi yako. Yaani hata kule kwenye
kutokufanya jambo pia ni uamuzi. Kwa maana hiyo ni kwamba kufanya na
kutokufanya ni uamuzi. Ndio hivyo hivyo pia katika kuamua kuwa mfuasi au
kiongozi.
Na wengi kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa na
maswali mbalimbali kuhusiana na uongozi. Maswali kama vile ; nini ninachohitaji
kuwa nacho ili niweze kuwa kiongozi? uongozi una sifa zipi na ni yapi majukumu
ya kiongozi? Mimi kama kiongozi nitaweza vipi kuwaongoza wale waliopo chini yangu? Hayo ni baadhi tu
ya maswali machache ambayo wengi wamekuwa wakijiuliza.
Ila ningependa kukwambia tu kwamba kabla haujafikiria
au kuwa na wazo la kutaka kuwa kiongozi ni muhimu kwanza ukajifunza kujiongoza
wewe binafsi. Kuwa na nidhamu binafsi ni
jambo la muhimu sana katika uongozi, Kwani Kamwe hautoweza kuja kufanikiwa katika
kuwaongoza wengine katika jambo lolote ikiwa wewe mwenyewe unashindwa
kujiongoza. Na kama tujuavyo kwamba; maisha yetu kwa kiasi kikubwa yamekuwa
yakiongozwa zaidi kutokana na ushawishi
tunaoupata kutoka kwa jamii zetu na mazingira yetu kwa ujumla. Kwa hiyo, kabla
haujafikiria kuwa kiongozi ni muhimu ukafanikiwa kwanza kujiongoza mwenyewe halafu
uwe na ushawishi mkubwa kwa wale unaowaongoza , sababu watu hao watakuwa
wanafuatilia sana kile utakachokuwa unakifanya ama kukitenda. Na Ikiwa utendaji
wako utakuwa mzuri, basi hata utendaji kazi wa wale unaowaongoza utakuwa mzuri
pia. Na ikiwa utendaji wako utakuwa mbaya basi tegemea kukutana na hali hiyo
hiyo pia kutoka kwa wale waliopo chini yako. Unatakiwa uongoze kwa mfano, kwani
hakuna aliye tayari kuongozwa kufanya jambo ambalo kiongozi wake halifanyi. Na
sababu kubwa hapo ni kama nilivyokuambia awali kwamba maisha yetu kwa kiasi
kikubwa yanaongozwa zaidi na ushawishi tunaoupata kutoka kwa jamii zetu pamoja
na mazingira yanayotuzunguka. Iwe kwenye maisha binafsi, kikazi, mahusiano,
ndoa, biashara n.k inakupasa ujiongoze mwenyewe kwanza kabla haujafikiria
kumwongoza yeyote yule ili uweze kupata ufanisi au matokeo yaliyo bora kutoka
kwa yule unayemwongoza.
Unahitaji kuwa na ujuzi kuhusiana na masuala
ya uongozi ili kuweza kuwa kiongozi bora na sio bora kiongozi. Kwani wengi
wanaojiingiza katika masuala ya uongozi mara nyingi huwa wanakosa ujuzi katika
kujiongoza wao binafsi au kikundi fulani na matokeo yake kusababisha kuanguka
kwa wao binafsi, kikundi kinachowaongoza, mashirika, taasisi na kufikia hatua
ya kushindwa kufikia lengo tarajiwa. Ebu tuangalie sababu inayowafanya wengi
wasiwe na ujuzi katika uongozi.
Kwa
nini baadhi ya watu wana ujuzi katika uongozi huku wengine wakiwa hawana?
Hilo ni swali ambalo limekuwa likigonga
vichwa vya watu wengi kwa muda mrefu sasa na ikiwezekana wewe ukiwa ni
mmojawapo. Kwani kuna uwezekano ukawa
umekwishawahi kujiuliza swali la aina hiyo hapo kabla. Na jibu la swali
hilo ni kwamba; uongozi ni ujuzi ambao hatuzaliwi nao. Huu ni ujuzi ambao
unaweza ukauendeleza na hata kufuzu. Japokuwa kuna uwezekano wa uwepo wa watu
wenye vipaji sana linapokuja suala la kuwa kiongozi, lakini jambo la muhimu
unalopaswa kulitambua na kulizingatia ni kwamba kila mtu anaweza kuwa kiongozi.
Ni maamuzi yako tu ya kuamua kuinuka ili
kupata uzoefu zaidi pamoja na hekima katika uongozi. Jifunze kadri uwezavyo
kuhusiana na uongozi na tumia kile utakachojifunza kisha kuwa utahayari wa
kuendeleza kile unachojifunza, na matokeo ya wewe kufanya hivyo ni kuja kupata
uzoefu pamoja na hekima katika suala zima la uongozi.
Pia ni lazima ujifunze na utambue wewe ni
aina gani ya kiongozi. Unaweza kufahamu
wewe ni kiongozi wa aina gani kwa kujitazama wewe binafsi, kwa kuangalia kile
unachokifanya au kinachokupa hamasa ili
uweze kujitengenezea nembo yako (brand) .Kwani kuwa na nembo katika zama hizi ni
jambo la muhimu sana. Na ninapozungumzia
nembo, nakuwa nazungumzia utambulisho wako. Yaani ujulikane kama kiongozi wa
aina gani? Kwa mfano; unaweza ukajulikana kama kiongozi wa masuala yahusuyo siasa, elimu, maisha, dini n.k.
Watu wengi katika zama hizi wamekuwa sio
viongozi na badala yake wamegeuka kuwa kundi la wafuasi, na wameacha kabisa
hata kushika hatamu juu ya maisha yao. Yaani wamekubali kabisa kuamriwa jinsi
gani wanapaswa waishi maisha yao, na wala
sio watakavyo au wapendavyo wao. Na wengi wamekwenda mbali zaidi kwa
kukubali kila jambo linalowatokea katika maisha yao kuwa ni sawa ajari.
Mafanikio katika maisha sio ajari bali ni matokeo ya kile unachokifanya siku
zote za maisha yako iwe kwa kujua ama kutokujua. Wewe ndiye dereva mkuu wa
maisha yako. Kwa hiyo yaongoze maisha yako kuelekea kule unapotaka yawe, na
uamuzi ni wako na si wa mwingine kubali au kataa. Hilo ni kosa ambalo wengi
wamekuwa wakilifanya kwa miaka kadhaa sasa kwa kuruhusu wengine wayatawale
maisha yao huku wakishindwa kutambua jinsi gani linawagharimu maisha yao .Hilo
ni kosa ambalo hupaswi kulifanya rafiki.
Ikiwa unataka kuchukua utawala juu ya maisha
yako na kuweza kuvifikia vipawa vingi
vilivyopo ndani yako ( wewe una uwezo mkubwa sana uliopo ndani yako) basi
nakushauri tu rafiki yangu uchukue hatua mara moja katika kumwendeleza kiongozi
aliyepo ndani yako. Tunahitaji kuwa na
viongozi wengi katika jamii zetu. Sasa la kujiuliza hapo ni je, upo tayari kuwa
kiongozi ajaye?. Jibu la swali hilo unalo mwenyewe.

Post a Comment