HILI NDIO TAMKO LA CUF BAADA YA PROF LIPUMBA KUCHUKUA OFISI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kimepokea kutoka Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na Ushauri wa
Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa
Baada ya kupokea Ushauri huo, The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kinapenda kueleza yafuatayo:
1. Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act, No. 5 of 1992)
haimpi mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa
ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi
ya vikao vya Chama.
2. Msimamo huo wa kisheria wa nchi hii umetiliwa nguvu na kuthibitishwa
na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UAMUZI wa
tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela
na Magnus Msambila v/s Registrar of Political Parties & Others
(Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo aliamua kwamba:
“… I do not see anywhere in the Political Parties Act where the
Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties
or decisions that they make.”
Tafsiri ya uamuzi huo ni kwamba, “… Sioni popote katika Sheria ya Vyama
vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya
vyama vya siasa au maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya.”
3. Kwa msingi huo, CUF hatukuomba ushauri kwa Msajili na hivyo tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe.
4. Kwa msingi huo huo, tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote
kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri
yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya
siasa na na kuyatolea uamuzi. Uwezo huo ni wa Mahakama. Hivyo tunawataka
wanachama wa CUF na wananchi wote kupuuza ushauri huo wa Msajili na
wamwachie mwenyewe ndoto zake na propaganda za kitoto.
5. Ni fedheha na aibu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa mwenye hadhi ya
Ujaji kukubali kutumiwa kiasi hicho na kushindwa hata kufanya rejea
kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu tulioutaja hapo juu ambao umeweka bayana
kwamba hana madaraka na uwezo aliojifanya anao. Itakumbukwa kwamba
Wabunge wa CUF walifanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma
tarehe 15 Septemba, 2016 na kumtahadharisha Msajili asikubali kutumiwa
kufanya alichokuwa anatakiwa kukifanya. Ni bahati mbaya sana kwamba
amefanya kile kile ambacho Wabunge wa CUF walieleza kwamba walikuwa na
taarifa kuwa ameagizwa kukifanya.
6. Tunajua kwamba baada ya hatua hiyo ya Msajili kufanya kazi asiyo na
uwezo wala mamalaka nayo na katika kutimiza malengo ya wanaotuma, mchana
wa leo Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake cha wahuni
kimevamia Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam na kupiga watu na
kufanya uharibifu wa mali. Tunamwambia Msajili wa Vyama vya Siasa
atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na yatakayofanywa na kikundi
hicho ikiwemo watu watakaoumizwa na uharibifu wa mali utakaofanywa kutokana na tamko lake hilo ambalo halina msingi wa kisheria.
7. Tunatambua yote haya yanafanywa kwa sababu watawala wameingiwa kiwewe
kutokana na hatua kubwa ambazo zimefikiwa na CUF katika kupigania haki
yake ya ushindi ulioporwa katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25
Oktoba, 2015. CCM haijakaa sawa tokea iliposhindwa vibaya na CUF katika
uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani mwaka 2015 na sasa imepata
mfadhaiko kutokana na jinsi jumuiya ya kimataifa ilivyosimama kidete
kutetea maamuzi hayo ya
kidemokrasia na haki za binadamu za Wazanzibari na Watanzania kwa
ujumla. Ni vyema watawala na kibaraka wao Prof. Ibrahim Lipumba na
kikundi chake pamoja Msajili anayewatumikia wakatambua kwamba CUF
haiyumbishwi na michezo yao ya kitoto na itaendelea kusimamia malengo
yake ya kupigania haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar na
Tanzania kikamilifu.
8. Chama kinasisitiza tena kwamba maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa
Taifa wa tarehe 21 Agosti, 2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
tarehe 28 Agosti, 2016 ni halali na yako pale pale na kwamba Prof.
Ibrahim Lipumba si Mwenyekiti wa CUF na wanachama waliosimamishwa au
kufukuzwa wataendelea kubakia wamesimamishwa au kufukuzwa isipokuwa tu
iwapo vikao vya Chama vitakapofanya maamuzi mengine.
9. Chama kinawataka viongozi wake wote na wanachama wake katika ngazi
zote kuanzia Taifa hadi Tawi kuendelea na kazi zao za ujenzi wa Chama
kama kawaida na kuendelea kufuatilia harakati za Chama chao kupigania
ushindi wetu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
HAKI SAWA KWA WOTE
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU - CUF

Post a Comment