VITENDO NDIYO CHANZO CHA MAFANIKIO
Kila mtu amekuwa akitaka
kufanikiwa, zunguka leo mitaani kila mtu anaimba wimbo mafanikio, ama kwa
hakika kama wimbo huu mafanikio ungekuwa unasikiliza waimbaji hawa wenye sauti
nzuri, wenye kujua kuyapangilia maneno yao wakati wanauimba wimbo huu mafanikio
basi huyu bwana mafanikio angekuwa ameshawapatia hayo mafanikio. Lakini habari
mbaya kwa waimbaji hawa ni kuwa wanamwimbia mafanikio ambae kila siku wanaishi
nae, wanatembea nae na kula nae yaani kwa kifupi wapo nae kila siku ila
waimbaji hawa hawalitambui hilo.
Kila mtu amekuwa akitaka
mafanikio lakini wanaofanikiwa ni wachache, ulishawahi kujiuliza kwa nini
pamoja na watu wengi sana kuyataka mafanikio hawayapati ni kwa sababu wanakosa
kitu kimoja kikubwa ambacho ndio nguzo kubwa ya mafanikio na msingi mkubwa wa
mafanikio na kitu hicho sio kingine bali ni vitendo. Mafanikio huja kutokana na
vitendo yaani vitendo au matendo ndipo mafanikio hupatikana. Ndio maana hata
katika biblia imeandikwa imani bila matendo imekufa, wakiwa na maana kuwa
huwezi kusema una imani bila kutenda imani hiyo.
Leo watu tumekuwa
tukitaka mafanikio lakini hatutaki kutenda vile mafanikio yanataka, leo hii mtu anakuambia nataka kuwa
daktari lakini mambo anayofanya hayaendani kabisa na huo udaktari anaousema.
Kutokana na kuwa vitendo huleta mafanikio ndio maana watu husema kuwa ni kufanya yaani huwezi kuwa mtu
fulani kama hujafanya kile kitu. Katika hili pia biblia imesema “atafutae
atapata na abishae atafunguliwa”. Hivyo huwezi kuwa mtu fulani kama hujatenda
lile jambo.

Kama unataka kuwa
mkulima ni lazima uanze kulima ndipo utakuwa mkulima, huwezi kuwa
mfanyabiashara kama hujaanza kufanya hiyo biashara, huwezi kuwa mwandishi kama
hujaanza kuandika. hivyo kuwa ni kufanya na kufanya ndio mafanikio. Watu wengi
sana tumekuwa hatupati maendeleo kwa sababu tu matendo yetu yamekuwa hayaendani
na mafanikio hata kidogo.
Leo hii utamkuta kijana
anapiga kelele kuhusu mafanikio lakini hataki kufanya kazi kwa bidii anafanya
kazi ilimradi tu anafanya kazi yaani yupo yupo tu hana mpangilio wowote katika kazi
yake. Leo hii kutokana na sera ya serikali ya awamu ya tano hapa kwetu Tanzania
ukipita huko mtaani wimbo unaoimbwa ni “hapa kazi tu”, lakini jambo ambalo
linakuja kushangaza na pengine kuacha viulizo vingi sana maishani ni pale
unapokuja kugundua kuwa idadi kubwa ya wale wanaosema hapa kazi tu ndio wasio
na kazi wapo wapo tu. Yaani kinachotokea ni kuwa wapo tayari kutamka neno kazi
lakini hawapo tayari kufanya kazi hizo.
Swala la kukosekana kwa
vitendo linajidhihirisha hata katika elimu ambapo watoto wetu, wadogo zetu na
wazazi pia tunakosa vitendo katika elimu. Utakuta mwanafunzi anataka afaulu,
tena kwa alama za juu lakini mwanafunzi huyu huyu hafanyi juhudi zozote katika
masomo yake husika badala yake anaenda shuleni kwa kuwa tu anapaswa kwenda.
Wazazi nao wanataka watoto wao wafanye
vizuri katika elimu lakini wanachofanya ni kulipa ada tu, yaani wao wakishalipa
ada basi wanahisi kuwa wamemaliza mchango wao katika elimu jambo ambalo sio,
mwanao anahitaji toka kwako vitu vingi na sio ada tu.
Leo hii lazima utambue
kuwa vitendo ndio msingi wa mafanikio kama ilivyo katika kukata njaa au kiu ya
maji. Huwezi kushiba ikiwa hujala, kiu yako ya maji haiwezi kuisha ikiwa
hutokunywa maji. Hivyo tambua kuanzia leo hii usiishie tu kuongea bali toka
ukatende na hapo ndipo mafanikio utayaona, kumbuka kuwa ni kufanya.
Nikutakie kila kheri
katika kuanza vitendo leo hii.
Post a Comment