Header Ads

Kwanini Unajilaumu Katika Haya Na Bado Hubadiliki?

            Habari mpenzi msomaji wa makala hii ndani ya blog ya mtegagachemit.blogspot.com,awali ya yote tumshukru sana mwenyezi Mungu kwa kutulinda na pia kuweza kutukutanisha mahali hapa kwa mara nyingine ili tuweze kuendelea kuongeza maarifa madhubutu kabisa yanayolenga kuboresha maisha yetu.
Katika siku ya leo napenda kukushirikisha baadhi ya mambo ambayo tunayafanya na kisha kujilaumu lakini bado tunaendelea kuyafanya bila kubadilika,utakuta mtu anajuta kwa kufanya jambo fulani akisema sitarudia tena lakini muda kitambo kidogo tu unamkuta anajuta tena pengine katika jambo lile lile alilokwambia hatodhubutu kulirudia kulifanya.Je wewe ndugu yangu anguko la kujuta kwako liko wapi?Haya ni baadhi tu ya maanguko tunayokabiliana nayo kwenye maisha yetu ya kila siku:-

1. Katika matumizi ya muda;Muda ni rasilimali ambayo mwenyezi Mungu ametugawia kwa usawa bila upendeleo kwa watu wote iwe maskini au tajiri wote wana muda sawa,kinacholeta tofauti ni katika matumizi ya muda huu,kila mtu anapanga yeye mwenyewe muda wake autumiaje.Pamoja na uhuru huo wa matumizi ya muda wengi wetu tunakutana na changamoto na nidhamu ya matumizi ya muda wetu,mfano mimi mwenyewe nilikuwa na najilaumu sana ninapopanga kuwahi kuamka saa kumi na moja kila siku,wakati mwingine najikuta na uchovu sana najiambia acha nilale kidogo tu,nakuja kushutuka kumekucha na ratiba yangu imevurugika,kinachofata naanza kujilaumu kwa kwanini nisingeamka tu muda ule,najiambia sirudii tena kosa hili,lakini baada ya siku kazaa najikuta narudia tena,hili si kosa tena bali ni anguko la majuto yangu kwa sababu nimeshindwa kubadili toka katika kosa la kwanza ingawa niliweza kuishinda hali hii kwa kuwa gaidi wa kusimamia nilichokipanga,jiulize nawe ndugu yangu umekutana na majuto haya mara ngapi? Chukua hatua ya kigaidi sasa nawe kwa kuacha demokrasi ya kivivu inayokuletea majuto kila mara.

2. Matumizi mabaya ya pesa zako;Hili ni janga kubwa sana linalokumba jamii yetu kwa kiwango kikubwa sana,sababu kuu ukosefu wa maarifa yahusuyo fedha kwenye jamii ,elimu hii haipo katika mtaala wetu wa masomo ya lazima kutoka shuleni.Hali hii huchochewa na nidhamu mbovu ya matumizi ya pesa zetu,huwa tunalalamika sana kwa kutumia kauli hii ”mbona napata pesa nyingi sana lakini sielewi zinapotelea wapi?” Hapa ndo kwenye ugonjwa mkubwa sana,tuna desturi ya kutathimini matumizi yetu ya pesa baada ya kuishiwa pesa kwenye akiba zetu.Jambo la msingi hapa tunatakiwa kuwa na mpangilio thabiti wa vipato vyetu tena kwa maandishi na kuvifata kwa nidhamu ya hali ya juu sana,hakikisha kila shilingi inayotoka mfukoni mwako haikiuki mpango wako wa kifedha.Kinyume na hapo kilio kile kile kitaendelea kwenye maisha yako,na kujilaumu itakuwa jadi yako pia,ebu jiulize swali hili msomaji wangu,je mimi napenda kujilaumu kila wakati? Kama jibu nihapana basi chukua hatua ya mabadiliko,na kama jibu ni ndiyo nakupa hongera pia kwa kuendelea na utaratibu ulionao wa kuendelea kujilaumu,ni vyema ukabadili yale yaliyo chini ya uwezo wako kama kweli huyafurahii kwa dhati.

3. Kushindwa kutimiza malengo yako; Katika maisha yetu ni muhimu kujiwekee malengo yako tena makubwa kiasi cha kukufanya uhamsike kila wakati,pamoja na hayo kuna msemo unaojulika sana usemao”mipango si matumizi”,nami napenda kukwambia kuwa kama kujadhamiria kwa nia ya dhati katika kuyafikia malengo yako,hakika utaendelea kuugua ugonjwa huu wa kujilaumu kila mwaka bila mabadiliko yoyote,utakuwa mtu wa kuhamisha malengo yale yale mwaka hadi mwaka bila mafanikio.Napenda nikupe changamoto nyingine msomaji wangu,ebu jiulize kweli unataka mafanikio na unachukia hali yako uliyonayo sasa? Kama jibu ni kweli,huu ndo wasaa wa kubadili maisha yako,pata muda wa kutafakari anguko lako liko wapi,anza kufanya usafi wa anguko hili,kama liko kwenye tabia anza kuibadili taratibu,ila kumbuka lazima uilipe gharama ya maisha haya unayoyataka kuyaishi,kama unataka utajiri lazima uanze kuishi kitajiri kabla ya kuwa tajiri tofauti na hapo hadithi itaendelea kuwa ile ile mwaka hadi mwaka!

Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo unatakiwa uyabadili msomaji wangu ili uondokane na hali ya kujilaumu na huku ukiendelea kuanguka kwa jambo lile ambalo hupendi litokee tena.Waweza kutumia kauli iliyosheheni mtaani sasa ya kutumbua majipu,jikague wewe mwenyewe katika mfumo wako mzima unaoutumia kuishi kila siku,anagalia ni mambo gani yanayokukwamisha kusonga mbele,iwe ni madeni,marafiki,kazi uliyoichagua n.k,hayo ndiyo majipu yako,anza kuyatumbua mara moja bila kusita hata kidogo.

No comments

Contact us:Email:godfreymtega@gmail.com/WhatsApp-+255758297744/+255716824009 . Powered by Blogger.