HISIA ZAKO ZIMEFICHA UFUNGUO WA MAFANIKIO YAKO
Binadamu yeyote ana kawaida ya kuwa na “hisia”. Na kuwa binadamu maana yake ni kuwa na hisia. Ukweli ni kwamba, watu wote tunapata hisia tofauti na ni za kila aina; mfano ni kama kuwa na upendo, furaha, chuki, hasira, kujisikia vibaya na mengine mengi. Kwa maana nyingine, watu wote tuna hisia zinazofanana, lakini kinacholeta tofauti na kila mmoja wetu kuonekana wa kipekee ni namna tunavyochukua hatua dhidi ya hisia, pindi zinapotujia. Linapokuja suala la kuwekeza pesa, katika mazingira ambayo tunahisi uwezekano wa kupoteza (risk), watu wote huwa tunapata “Hofu” na hii ipo hata kwa watu waliofanikiwa. Tofauti iliyopo ni jinsi gani kila mmoja wetu anavyoweza kumudu hofu inayomkabili kwa wakati huo.
Kwa watu walio wengi, hisia za hofu ndizo hutengeneza fikra au mawazo juu ya utumiaji wa pesa. Kwa mfano: watu wengi wana mawazo ya kuitunza pesa katika sehemu salama kwa malengo ya kuzuia upoteaji wake na kudhibiti isihishe”. Watu wa namna hii siyo rahisi kuonyeshwa fursa ya biashara na wakaweza kuichangamkia, kwa sababu kila mara wanakaa wanafikiria jinsi pesa yao itakavyo potea pindi wakiitoa pale walikoitunza. Kwa hiyo, kwao kuwekeza pesa ambayo itarudi baada ya muda mrefu (mwaka au zaidi), wao tayari wanapata hisia ya kwamba tayari imepotea na hivyo kushinikizwa na nguvu ya hisia zao kutoachia pesa hiyo waliyonayo tayari. Lakini, watu waliofanikiwa, hofu ya kupoteza pesa ndiyo huwafanya kuwa makini katika kutumia pesa. Kutokana na kuwa makini, watu hawa hulazimika kujifunza njia bora zaidi juu ya utumiaji na uwekezaji wa pesa, ikiwa ni pamoja na mbinu za kukabiliana na changamoto za kiuwekezaji. Kwa ujumla, watu wote tunaweza kuwa na hisia sawa, lakini tukawa na mawazo au fikra tofauti: Maana yake ni kwamba, tofauti iliyopo juu ya fikra zetu, ndiyo husababisha tofauti ya mambo tunayofanya na tofauti ya mambo tufanyayo ndiyo mwisho wake huleta matokeo au vitu tofauti tulivyonavyo.
Katika kuwajibika kwa hisia zetu ndiyo sababu tunafanya mambo tofauti kabisa na pia tunakuwa na mafanikio tofauti ya kipato. Katika kufanya uchunguzi wa kina, nimegundua kwamba, sababu kubwa inayosababisha watu wengi tuhangaike kutafuta kipato ni “hofu ya kupoteza pesa”. Hofu ya kupoteza pesa, mara nyingi huwafanya watu kufanya vitu vidogo vidogo, ambavyo mara nyingi uhitaji kuwekeza pesa kidogo sana. Na endapo ikitokea fursa yenye kuhitaji kiasi kikubwa cha pesa, watu wengi hushindwa siyo kwa sababu hawana pesa hiyo bali ni ile hofu ya kupoteza/kupata hasara. Hofu hii ikisha kuwa kubwa, basi hisia zinakutuma kutofanya au kuacha kuendelea na fursa hiyo. Hofu ya kupoteza pesa pindi unapoiwekeza ndiyo inawafanya watu wengi waliosoma kupendelea ajira kwa sababu, ukiwa na ajira, haulazimiki kuwekeza pesa yako, badala yake wewe unakuwa ni wa kupokea mapato (mshahara), licha ya kwamba unachokipokea hakikidhi mahitaji na hivyo kuendelea maisha ya kuhangaika siku hadi siku.
Katika kitabu cha “Emotional Intelligence” ambacho kimeandikwa na bwana Daniel Goleman; anaeleza na kufafanua kwa nini watu wengi wanaofanya vizuri shuleni ni nadra sana kufanya vizuri katika maisha halisi ya ulimwengu. Jibu la mwandishi ni kwamba, nguvu ya hisia uliyonayo ni kubwa kuliko uwezo wa darasani au elimu kutoka mfumo rasmi. Ndiyo maana, watu wanaothubutu, wanaofanya makosa na kuyasahihisha, mara nyingi wanafanya vizuri zaidi kuliko watu ambao walijifunza kutokufanya makosa shuleni na hawa wanaogopa sana kuthubutu. Watu wanaothubutu kwa maana ya kuchangamkia fursa wanafanya hivyo bila kujali changamoto ambazo zinaweza kujitokeza mbele ya safari. Uhuru wa kipato unakuja pale unapoanza kujisikia huru kufanya makosa, kujifunza na kuvumilia mpaka malengo yako uliyokusudia yatimie.
Baada ya kusoma kitabu cha “Goleman”, nilikuja kugundua kuwa suala zima la kupata mafanikio ya pesa linachukua asilimia 90% ya mchakato huo ni hisia na asilimia 10% ni taarifa za kitaalam juu ya kipato na pesa (unajifunza shuleni). Mwandishi “Goleman”, akimnukuu Erasmus wa Rotterdam katika karne ya 16, anatumia uwiano wa 24:1, katika kuliganisha nguvu ya ubongo wa hisia na ubongo wa uhalisia. Kwa maneno mengine, anasema pale hisia zinapokuwa juu, basi uwezo wa kufikiri mambo halisi unakuwa chini. Wote tumekutana na matukio katika maisha, pale hisia zetu zilipozidi zile za fikra sahihi, mara nyingi, ilionekana dhahiri kuwa nguvu ya hisia ilishinda nguvu ya fikra sahihi.
Ndiyo maana linapokuja suala la pesa, hisia zetu mara nyingi huwa zinatukamata kweli kweli; kiasi kwamba, unaweza kukuta mtu anajua ni nini anatakiwa kufanya, lakini anafanya kile anachojisikia kufanya—na mara nyingi tunachukua mkondo ule tunaodhani ni salama. Kwa mfano: kila mmoja wetu anajua kuwa, ili upate pesa ni lazima ufanye kazi kwa bidii sana, lakini hisia zetu zinatwambia kuwa kazi ni ngumu, inapoteza muda n.k. Mtu huyo huyo anayedai kuwa kazi fulani yenye kuingiza kipato ni ngumu au inahitaji muda mwingi ndiye unamkuta ni kinara wa kuangalia runinga, kuchati (Facebook n.k), kwenda kwenye vikao vya harusi na mengine mengi. Kwa maana nyingine, mtu huyu hisia zake ni kubwa kuliko fikra sahihi kama “kufanya kazi kwa bidii ili kupata pesa”.
Sehemu ya kufanikiwa kimaisha ni pamoja na kutambua mwenendo wa hisia zinazokurudisha nyuma , na kuchukua hatua ili kudhibiti mwenendo wa hisia hizo. Pale tunapokabiliwa na hofu ya kupoteza pesa ni lazima tuhakikishe wote kwa husahihi tunazitambua hizo hofu zinazotokana na hisia, kabla hazijawa na nguvu ya kutushinda kuziondoa. Hii inahitaji uelewa binafsi wa kuweza kujitambua na uelewa huu unatokana na kujifanyia tathimini binafsi muda wote. Kama ukijitahidi kudhibiti hisia zako na ukajikita katika kufanya vitu ambavyo unajua fika kuwa ni sahihi kuvifanya, basi una nafasi nzuri sana ya kuweza kupata mafanikio makubwa. Ni mchakato wa kufahamu na kujua ni fikra zako zipi ni hisia na zipi ni sahihi. Na mjadala ambao ni muhimu kwako ni ule unaoufanya wewe peke yako, yaani wewe na nafsi yako.
Unapokuwa unashughulika na hisia zako, mara nyingi ni vizuri kuwa na mtu maalum wa kuongea naye, ili kupata ushauri wa maana. Unapokuwa karibu na mtu huyu ambaye ni kama kocha wako anakuwa karibu sana na wewe, huku akijitahidi mara kwa mara kukumbusha kitu unachotakiwa kukifanyia kazi. Mwongozo wake utakufanya uzidi kwenda mbele. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwa na makocha mbalimbali, ambao wako tayari kutoa muda wao kwaajili ya mafanikio yako.
Post a Comment