SHIRIKA LA MAGEREZA KUSHIRIKIANA NA KAMPUNI YA KICHINA KWENYE KILIMO CHA KISASA
Kamishna Jenerali wa Mgereza – CGP John Casmir Minja(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawekezaji wa masuala ya Kilimo cha kisasa mara baada ya mazungumzo Ofisini kwake leo Novemba 2, 2016, Makao Makuu ya Magereza(kulia) ni Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya CAMCE kutoka nchini China Bw. Lane Lei(kushoto) ni Mwakilishi wa Kampuni ya Wazawa ya KG CORPORATION Bw. Dan Ngowi.
Na; Lucas Mboje, Jeshi la Magereza – Dar es Salaam
KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, John Casmir Minja amekutana na Wawekezaji wa Kampuni ya CAMCE kutoka nchini China pamoja na Kampuni ya Wazawa ya KG CORPORATION na kumuahidi kushirikiana na Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza(Prisons Corporation Sole) katika kuwekeza katika miradi mbalimbali ya Kilimo cha kisasa, Madini na Viwanda vinavyoendeshwa na Shirika hilo.
Akizungumza na Wawekezaji hao leo asbuhi Ofisini kwake (Jumatano, Novemba 2, 2016) alisema kwamba Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake la Uzalishaji mali lina fursa nyingi za miradi ya uwekezaji kwenye sekta nyingi kama vile Kilimo, Viwanda na Madini ambapo aliwahahakishia ushirikiano wa kutosha kwenye uwekezaji wao.
Wawekezaji hao tayari wamefanya mazungumzo na Viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo wanatarajia kuiingia Makubaliano (MoU) na Jeshi la Magereza kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ya Kilimo cha kisasa katika Gereza Idete lililopo Mkoani Morogoro pamoja na Mradi wa Ngo’mbe wa nyama Gereza Ubena, Mkoani Pwani.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya CAMCE kutoka nchini China Bw. Lane Lei alisema amefurahishwa na ziara waliyofanya nchini na wapo tayari kuwekeza hapa Tanzania.
Naye, Mwakilishi wa Kampuni ya Wazawa ya KG CORPORATION Bw. Dan Ngowi ambayo inashughulikia na masuala ya Kilimo cha mazao ya chakula na nyama alisema watawekeza kwenye kilimo hususan cha umwagiliaji na watajenga Kiwanda kwa ajili ya usindikaji.
Shirika la Uzalishaji mali la Magereza(Prisons Corporation Sole) lina jumla ya Miradi 23, kati ya hiyo miradi 15 ni ya kilimo na mifugo na 8 ni ya viwanda vidogo vidogo, pia zipo shughuli za mradi wa Kikosi cha Ujenzi zinazosimamiwa na Shirika hilo.
Mkakati wa Jeshi la Magereza hivi sasa ni kuendelea kuboresha maeneo mbalimbali pamoja na kuchangamkia fursa zilizopo ikiwemo uwekezaji wa ubia kwenye miradi yake ili kuhakikisha kuwa linafikia ufanisi unaotarajiwa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mwisho.
Post a Comment