NA MWALIMU ERICK SHIGONGO:RAFIKI ANAWEZA KUWA KIKWAZO CHA WEWE KUFANIKIWA
Unaweza ukawa na kiu ya kufanikiwa, tena sana, ukapambana sana na ukaona kwamba unakwenda kufanikiwa lakini kukatokea mambo fulani yakakufanya ukashindwa kufanikiwa.
Ndugu yangu! Watu wengi hawafanikiwi kwa sababu ya MARAFIKI. Tumewapa kipaumbele marafiki zetu, wakati mwingine tunasema kwamba wamekuwa mabesti sana kama ndugu lakini kumbuka kwamba unapochagua marafiki ambao si sahihi, unaweza kupotea, yale mafanikio ambayo yanakunyemelea yakapotea.
Unaposema fulani ni besti wangu, inamaanisha kwamba akikwambia twende huku, unakwenda, si ndiyo? Na akikwambia tufanye hivi unafanya, si ndiyo? Wakati mwingine hata kama kitu hutaki kufanya, utajikuta ukifanya kwa sababu rafiki yako kakwambia, unaona ukikataa, utamkasirisha kitu ambacho hutaki kutokea.
Katika miaka 47 niliyoishi hapa duniani, nimeona watu wakipoteza mafaniko kwa ajili ya marafiki zao, nimewaona watu wakipoteza mali kwa ajili ya marafiki na pia nimeona ndoto za watu zikipotea kisa marafiki, unapochagua marafiki ambao si sahihi, una nafasi kubwa ya kupotea.
Hebu fikiria unakuwa na rafiki ambaye kila siku yeye ni stori za wanawake tu, wanaume tu, wapi tukale bata au kufuata wanawake wa aina gani, au wanaume mapedeshee! Hakuna hata siku moja ambayo amekaa na kuzungumza nawe kuhusu kufanikiwa, hajawahi hata kukwambia leo twende kwenye semina ya ujasiriamali tukamsikilize mwalimu ili tufanikiwe.
Kuna wengine, ukisoma meseji za marafiki zao, zinazungumzia starehe, kupata wanawake au wanaume, hakuna hata moja ambayo inayosema kwamba tufanye nini ili tufanikiwe.
Ndugu yangu, marafiki wa hivi hawafai hata kidogo. Wakati mwingine labda unaogopa kuwaacha, ila hebu kaa chini na fikiria kuhusu maisha yako ya mbele, je, ukiendelea nao utaweza kufanikiwa? Kama mtu anazungumzia wanawake au wanaume tu na viwanja vya starehe, je hiyo itaweza kukusaidia? Haiwezi hata kidogo.
Unachotakiwa ni kuwafuta marafiki wote ambao unaona hawana umuhimu, si dhambi kumfuta rafiki ambaye yeye stori zake ni starehe tu, unatafuta, kabla ya kufika huko, kwanza anza na marafiki zako.
Vijana wengi wanaogopa kuwafuta marafiki zao na ndiyo maana mwisho wa siku wanashindwa kufanikiwa. Marafiki wengine ni watu wa kutukatisha tamaa, unamwambia wazo zuri la biashara, badala ya kukutia nguvu kwamba utafanikiwa lazima ujaribu, yeye anakwambia kwamba hata baba yake aliwahi kufanya, akashindwa, mjomba wake alijaribu akashindwa, na hata yeye alijaribu pia akashindwa.
Ndugu yangu! Hakuna kitu kigumu duniani, jaribu, ukishindwa zaidi ya mara mia moja, jua kwamba hicho ni kigumu, siyo useme kigumu na wakati hujawahi kujaribu hata mara moja.
Marafiki wengine hawafai, tunapoanza kuwafuta marafiki tusiangalie ni nani! Tusiangalie kwamba yeye ni swahiba wangu wa ukweli, tusiangalie kwamba ni mtoto wa rafiki wa baba yangu, tunapoanza kutafuta mafanikio ni lazima tuondoe vikwazo vyote vitakavyotufanya turudi nyuma.
Huu ni mwanzo. Unasubiri nini kumfuta rafiki ambaye anaonekana hana msaada mkubwa katika maisha yako? Unasubiri nini kumfuta rafiki ambaye kila wikiendi anakwambia muende kula bata au klabu? Unasubiri nini kumfuta rafiki ambaye kila siku anakwambia mambo ya ngono tu? Unasubiri nini rafiki yangu? Au unataka mpaka uone madhara yake baadaye na useme ningejua?
Huu ni muda wa kuamua, ni muda wa kufanya maamuzi magumu. Najua marafiki wanatesa sana, najua marafiki wanaturudisha nyuma, katika safari ya kutafuta mafanikio hatutakiwi kusema kwamba huyu nilikua naye tangu utotoni, kwamba huyu alikuwa akinisaidia kipindi cha nyuma, tunapoamua kuwafuta marafiki, ni lazima tujue kwamba tunafanya uamuzi mgumu na wenye mafanikio makubwa sana katika maisha yetu. Futa marafiki wasiofaa na uache wale ambao unaamini ukiwa nao utakuja kufanikiwa.
Lifanyie kazi hilo na ninakuahidi utafanikiwa.
E.J Shigongo.
Post a Comment