Mpango wa kupeleka watu wakaishi Mars
- 29 Septemba 2016
Mjasiriamali Elon
Musk ametangaza mpango wake wa kuunda makao ya binadamu katika sayari ya
Mirihi (Mars kwa Kiingereza),ingawa wanaotaka kunufaika watahitajika
kulipa pesa nyingi.
Tiketi ya kusafiri hadi kwenye sayari hiyo inakadiriwa kugharimu takriban $200,000.Bw Musk, aliyeanzisha kampuni ya kibinafsi ya usafiri wa anga za juu kwa jina SpaceX, alitangaza mpango huo katika kongamano la kimataifa la wataalamu wa anga za juu (IAC) mjini Guadalajara, Mexico, Jumanne.
Mpango wake, unajumuisha mfumo wa usafiri ambao utaweza kusafirisha watu 100 hadi Mars, safari yote ikichukua siku 80.
Baadaye, safari hiyo inatarajiwa kuchukua siku 30 pekee.
Bw Musk amesema ili kufanikiwa na kuhakikisha gharama kwa kila mtu ni $200,000, basi lazima kuwe na njia ya kutumia tena mitambo ya uchukuzi itakayotumiwa.
Ili kufikisha watu milioni moja, Bw Musk amsema: "Ninataka watu watazame kwamba ni jambo linalowezekana, jambo tunaloweza kutimiza katika uhai wetu ... na kwamba yeyote anaweza kwenda huko akitaka."
Chini ya mpango wa SpaceX, safari ya kwanza ya kupeleka watu sayari hiyo itafanyika 2022.
Chombo cha kwanza kupeleka watu Mars Bw Musk anataka kukiita The Heart of Gold, jina linalotokana na chombo kinachozungumziwa katika kitabu cha Douglas Adams The Hitchhiker's Guide to the Galaxy.
Kitarushwa kutoka Kituo cha Anga za Juu cha Nasa cha Keneddy, sehemu 39, ambayo ndiyo sehemu iliyotumiwa kurusha roketi na vyombo vya anga za juu chini ya mpango wa Apollo.
Mwishoni mwa wiki, Bw Musk alitangaza kwamba majaribio ya kwanza ya roketi kwa jina Raptor ambayo itatumiwa kurusha chombo hicho pamoja na kifaa cha kuiweka kwenye mzunguko anga za juu (booster) yalifanyika.
Tangi la mafuta ya kifaa hicho limeundwa na kufanyiwa ajaribio na Bw Musk alionesha picha ya tangi hilo na wafanyakazi.
ITS kubwa zitaweza kubeba hadi abiria 200.
Mpango wote utafadhiliwa na faida kutoka kwa SpaceX.
Bw Musk anatazama mpango huo wa kupeleka watu Mars kuwa "ushirikiano mkubwa wa umma na sekta ya kibinafsi" na anasema "hivi ndivyo Marekani ilivyoanzishwa".
Vyomvo vya anga za juu vitatumwa kila baada ya miaka miwili Mars inapokuwa imekaribia sana dunia. Umbali kati ya sayari hizo mbili utakuwa kilomita 57.6 milioni mwaka 2018.
Sayari hizo zinapokuwa mbali sana, huwa umbali kati yake ni kilomita 400 milioni.
Miaka ya karibuni, umbali huo umepungua kufikia kilomita 100 milioni pekee.
Gharama ya kusafiri baadaye inaweza kushuka hadi kati ya $100,000 na $140,000.
Mtu akitaka kurejea duniani, ataweza kufanya hivyo "bila malipo".
Post a Comment