Header Ads

USHAURI; Hatua Tano(5) Za Kuanzisha Na Kukuza Biashara Kwa Wale Ambao Hawana Pa Kuanzia Kabisa.

Habari rafiki? 
Changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, hivyo ujanja siyo kuzikimbia changamoto, bali kukabiliana nazo na kuzishinda ili kuweza kusonga mbele zaidi. Hii ndiyo sababu kupitia AMKA MTANZANIA tuna kipengele cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia malengo makubwa tunayojiwekea kwenye maisha yetu. 

Karibu kwenye makala yetu ya leo ambapo tunakwenda kupeana ushauri juu ya changamoto zinazowazuia watu kuanza biashara. Kwa zama hizi tunazoishi sasa, biashara ni kitu muhimu mno, iwe umeajiriwa au hujaajiriwa, unahitaji kuanzisha na kukuza biashara yako ili kuweza kujitengenezea uhuru wa kifedha. Na siyo lazima uache kazi yako ndiyo uanzishe biashara, kama ambavyo nimeeleza kwenye kitabu hiki; BIASHARA NDANI YA AJIRA (bonyeza kukipata) unaweza kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa. 
 
KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Imekuwa ndoto ya wengi kuanza biashara, lakini maswali ya awali kabisa ni nifanye biashara gani? Nianzie wapi? Nipate wapi mtaji? Nipate wapi soko la uhakika? Sasa leo kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto, tunakwenda kuangalia pa kuanzia, namna ya kupata soko, mtaji na hata jinsi ya kuikuza biashara yako. kabla hatujaingia kwenye ushauri wenyewe, hebu tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili; 

Mimi ni mpambaji, nadarizi ila nasumbuliwa na mtaji na soko na ni mfugaji mzuri wa kuku wa mayai ila kwa sasa nipo nipo tu sijui hata pakuanzia naomba ushauri wenu na msaada wenu. Amina S. A

Hiyo ndiyo changamoto kubwa inayomsumbua msomaji mwenzetu, na nina hakika wapo wengi ambao wana changamoto kama hiyo. Swali ni je unatokaje hapo ulipo? Moja kwa moja tunakwenda kuangalia hatua unazoweza kuchukua, tukitumia mfano wa msomaji mwenzetu na mingine kwenye hali kama hizo. 

HATUA YA KWANZA; Anzia hapo ulipo, hiyo ndiyo biashara uliyonayo tayari. 

Kitu kimoja ambacho nataka kukuambia mwanzo kabisa ni kwamba hapo ulipo tayari una biashara, ni wewe kuijua na kuanza kuifanyia kazi. Je kuna kitu ambacho unapenda kufanya? Au kuna kitu ambacho una ujuzi nacho? Je kuna uzoefu wowote umepitia kwenye maisha yako ambao wengine hawajaupitia? Je kuna elimu uliyopata ambayo wengine hawana au wanaihitaji? Au je umeajiriwa au kuna watu walishakulipa kutokana na kitu ulichokifanya? Kama umejibu ndiyo kwenye swali lolote kati ya hayo hapo juu, basi tayari biashara unayo. 

Kwa mfano wa msomaji mwenzetu hapo juu, ana ujuzi wa kupamba na wa kudarizi. Tayari ana biashara, tena nzuri sana ya kupamba na kudarizi. Kwa mwingine inawezekana ni ujuzi wa afya, au kilimo. Mwingine anaweza kuwa anapenda kuandika, mwingine kuimba. Mwingine anapenda kufuatilia michezo, au kutumia mitandao ya kijamii. Vyote hivi unaweza kuvigeuza na kuwa biashara. 

SOMA; USHAURI; Kuanza Biashara Kwa Mtaji Kidogo, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuikuza. 

HATUA YA PILI; Angalia ni nani mwenye uhitaji wa kile unachofanya au unachotaka kufanya. 

Ukishajua kile ambacho unacho, ambacho ndiyo unakigeuza kuwa biashara yako, angalia ni watu gani watahitaji huduma au bidhaa yako. Angalia ni watu gani ambao wana shida au mahitaji ambayo wewe unaweza kuyatimiza kupitia kile ambacho unakifanya. 

Kwa msomaji wetu aliyetuandikia, wateja wake ni watu wanaofanya sherehe mbalimbali kama harusi au mahafali. Wateja wake pia ni watu wanaopenda mavazi yaliyodariziwa. 
Kama vitu unavyofanya wewe ni vingine, angalia watu gani wanaweza kunufaika navyo. 

Kama unapenda kufuatilia michezo, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika kupitia yale unayofuatilia leo. kama unapenda kutumia mitandao ya kijamii, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika kupitia wewe kuwa kwenye mitandao ya kijamii. Kama unapenda kuandika, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika na kile unachoandika. Kila unachofanya, wapo watu ambao wanakitafuta kwa hamu, ni jukumu lako kuwajua na kuwafikishia kile unachofanya. 

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuishinda Hofu Ya Kupata Hasara Kwenye Biashara. 

HATUA YA TATU; Wape watu kile unachotoa bila ya malipo. 

Hapa ninachukulia kwamba unaanzia chini kabisa, ambayo ni sehemu nzuri sana kuanzia kwa sababu sasa hivi huna namna ambavyo unatengeneza kipato. Hivyo unaweza kutoa huduma zako kwa wengine bila hata ya kulipwa. Kama unachotoa ni bidhaa basi anza kutoa kwa bei ya chini sana, ambapo hupati faida yoyote. Lengo ni watu wakujue wewe ni nani kwanza, hapo ulipo sasa hakuna anayekujua na hata ukiwaambia kuna kikubwa unaweza kufanya hakuna anayeweza kukuamini, hivyo unahitaji kujijengea uaminifu. 

Kwa msomaji mwenzetu aliyetuandikia hapa, anaweza kuanza kutoa huduma zake za upambaji bure kabisa. Angalia sherehe mbalimbali zinazofanyika pale unapoishi na omba kujitolea kupamba bure kabisa, wao wanunue tu mapambo. Au kama hizi hakuna, tafuta watu wanaofanya upambaji, ambao tayari wameshajijengea majina, waombe kujitolea kuwasaidia kazi bure kabisa, wasikulipe chochote. Lengo hapa ni wewe ujifunze, pamoja na kuwaonesha wengine kile ambacho unacho. Pia kwenye kudarizi hivyo hivyo, anza kudarizi vitu vya nyumbani kwako/kwenu na wasaidie watu kudarizi. Kadiri watu wanavyoona kazi zako ndivyo wanavyotaka kufanya kazi na wewe. 

Kwa shughuli nyingine kama uandishi, tafuta njia ya kuwafikishia watu maandishi yako kwa bure kabisa. Anza kwa kuwa na blog, na andika mara kwa mara, kwa kuanza fanya kila siku, andika hata kwa siku mara mbili au mara tatu, andika sana, andika vitu ambavyo mtu akivifanyia kazi maisha yake yatakuwa bora. 
Kama unachofanya ni kufuatilia michezo, anza kuwapatia watu uchambuzi wa ile michezo ambayo unafuatilia, toa historia za ile michezo ambayo unaifuatilia, hakikisha watu wanapotaka taarifa kuhusu michezo hiyo, wanakuja kwako kwanza. 

Hatua hii ya tatu ni hatua muhimu kwani hapa ndipo watu wanapokujua na kuanza kuwatengenezea utegemezi. Wafanye watu wakutegemee wewe kupitia kile ambacho unawapatia. Kumbuka kwenye hatua hii hakuna faida yoyote unayotengeneza, unatengeneza jina kwanza. 

SOMA; USHAURI; Biashara Unazoweza Kuanza Kwa Mtaji Wa Tsh Laki Mbili Na Kuweza Kufanikiwa. 

HATUA YA NNE; Anza kutoza gharama kwa wale wanaotaka zaidi ya unachotoa. 

Ukishatengeneza jina lako, na watu wakaanza kukutegemea kutokana na matokeo bora unayotoa, sasa unaweza kuanza kuwatoza watu kwa kile cha ziada wanachotaka uwafanyie. Ni wakati gani w akufanya hivi utaona tu inakuja yenyewe, watu wataanza kukuuliza wenyewe kama unaweza kuwasaidia kwenye mambo yao yanayohusika na unachofanya, na wao wenyewe watakuuliza wakulipe kiasi gani. Hii ndiyo hatua muhimu kwako kujenga msingi sahihi na imara wa kibiashara. 

Kwa mfano ambao msomaji mwenzetu ametuandikia, hapa ndipo unapoanza kutoa huduma yako ya upambaji kwa gharama. Hapa umeshatengeneza jina lako, umeshashiriki kwenye sherehe nyingi na watu wameanza kuambiana kuhusu wewe. Hapa umeshawaangalia wengine wanaofanya wana mapungufu gani na wewe unakuja na suluhisho bora kabisa. 

Kama ni uandishi watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwapa ushauri wa moja kwa moja, au kama kuna vitabu umeandika ambapo watu wanaweza kujifunza zaidi. Kama ni matumizi ya mitandao, watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwatangazia biashara zao kupitia mitandao ya kijamii. Kama ni ufuatiliaji wa michezo, watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwaelimisha zaidi kuhusu michezo hiyo, au kuwasaidia kutabiri michezo hiyo. Yapo mengi ambayo watu watahitaji kutoka kwako. 
Unapofikia kwenye hatua hii ya nne, unahitaji kuwa umepitia biashara za wengine na kuona ni vitu gani unahitaji kufanya tofauti ili uwe bora zaidi ya wengine. 

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kupata Mtaji Wa Kuanzia Biashara. 

HATUA YA TANO; Kuza biashara yako. 

Unapofika hatua hii ya tano sasa una biashara ambayo ina wateja, ambao wapo tayari kukulipa ili kupata bidhaa au huduma unayotoa. Hapa sasa ndiyo unaweza kusema una biashara, na unachohitaji kufanya hapa ni kuikuza biashara yako. unaweza kuona ndiyo sehemu rahisi, lakini ukweli ni kwamba hii ni sehemu ngumu, kwa sababu kila siku unahitaji kuja na mbinu mpya na bora za kukuza biashara yako. 

Katika hatua hii ndiyo unaweza kuchukua mkopo wa kibiashara, kwenye hizo hatua nyingine za nyuma kamwe usichukue mkopo, utajipoteza. Chukua mkopo ukishakuwa na biashara ambayo tayari ina wateja wanaokulipa kwa kile unachofanya. 
Hizi ndizo hatua tano muhimu ambazo mtu yeyote anaweza kuzitumia kutoka chini kabisa mpaka kufikia kumiliki biashara kubwa na yenye mafanikio. 


No comments

Contact us:Email:godfreymtega@gmail.com/WhatsApp-+255758297744/+255716824009 . Powered by Blogger.