Hatua Nne (4) Za Kuchukua Ili Kuendelea Kufanya Kile Unachokifanya Hata Kama Utakumbwa Na Magumu Kiasi Gani.
Habari za wakati huu
ndugu msomaji wa makala za mtandao huu, ni matumaini yangu kuwa unaendelea
vizuri. Karibu katika makala ya leo ambayo nataka nikushirikishe juu ya hatua
nne za kuchukua ili kuweza kuendelea kufanya kile unachokifanya hata kama
utakumbwa na magumu kiasi gani.
Mara nyingi binadamu
tumekuwa ni watu wenye kujishughulisha
na mambo mbalimbali, hii yote ni katika kuhakikisha kuwa tunajiletea
maendeleo ambayo tumekuwa tukiyataka, lakini wakati ukiendelea kupambana ili
kuweza kujiletea mafanikio husika kuna baadhi ya mambo ambayo yanaweza kwenda
ndivyo sivyo na hapa ndipo huwa panakuwa na shida kubwa kwani ni watu wachache
sana ambao huwa na moyo wa kuendelea na shughuli zao hata kama mambo
hayajawaendea vizuri. Kama na wewe ni mmoja wapo wa watu hao basi karibu
tujifunze leo hii nini tufanye ili kuweza kubaki na ile hali ya kufanya shughuli zetu pamoja na
magumu tunayopitia.
1. Fikira chanya, siku zote katika
maisha yako fikiri mambo chanya, kuwa na fikira kuwa jambo unalolifanya
linawezekana japo wengi wanaona kuwa haliwezekani, na namna mojawapo ya kuwa na
fikira chanya ni kwa wewe kuacha zile fikira za bendera fuata upepo. Yaani
usifanye kitu fulani kwa kuwa wengi wanafanya au usifikiri kwa namna fulani kwa
kuwa wengi ndivyo wanavyofikiri hapana badala yake wewe fikiri katika njia
nyingine ambayo ni chanya. Ukiwa na fikira chanya basi hii itakusaidia wewe
hapo kuweza kubakia katika shughuli husika.
2. Jua unachokitaka, hatua ya pili ya
kuweza kukusaidia wewe katika kuweza kubaki katika shughuli yako ni kwako wewe
kujua nini unataka. Hapa utahitajika kuelewa kwa undani ni nini unakitaka
kutokana na shughuli husika ambayo umekuwa ukiifanya au ambayo unaifanya, jua
unachokitaka kutokana na kuajiriwa kwako, jua unachokitaka kutokana na kuwa
mkulima, jua unachokitaka kutokana na wewe kuwa mfanyabiashara. Ukishajua
unachokitaka basi ama kwa hakika hutohama katika shughuli yako bali utabakia
katika shughuli husika siku zote.
3. Tengeneza mpango, shughuli nzuri na
yenye kupendeza ni ile ambayo inafanyika chini ya mpango fulani, yaani shughuli
iliyo katika mpango fulani yaweza kufanyika kiurahisi sana na kwa kuvutia
kuliko shughuli ambayo haijapangiliwa katika mpango wowote ule, ni muhimu kuanzia
sasa ukajifunza kupangilia shughuli zako ili tu uweze kuzifanya kwa ubora na
zikuvutie wewe mwenyewe. Kuna uwezekano mkubwa sana kuwa kuna baadhi ya watu
huondoka katika shughuli zao kwa kuwa tu hawajazipangilia vizuri hivyo
haziwavutii hata wao wenyewe na ndio maana huziona kuwa kama shughuli
zisizowafaa hata kidogo, kumbe shida haipo katika shughuli bali shida ipo
katika mpango wa shughuli husika, hivyo basi kuanzia leo hakikisha unapangilia
shughuli yako au zako katika mpango unaoeleweka vyema.
4. Fanya shughuli chache, usiwe mtu wa kufanya shughuli nyingi sana kwa wakati mmoja hii inaweza
kuhatarisha utendaji wako wa kazi na hatimae ukakufanya uondoke katika shughuli
fulani, hivyo basi hata kama una shughuli kubwa sana hebu anza kwa kufanya
shughuli ndogo ndogo ambazo zitakufanya uweze kutimiza ile shughuli kubwa.
Kutaka kufanya shughuli kubwa kwa wakati mmoja
wakati mwingine kwaweza kukufanya uone ni kama jambo hilo haliwezekani
na matokeo yake ukaamua kuacha kufanya shughuli husika lakini kwa kuchukua
hatua za kufanya shughuli ndogo ndogo ili kuweza kutimiza ile shughuli kubwa
kutakupa moyo wa kuendelea kutenda.
Nakutakia kila kheri
katika kuzifuata hatua hizi.

Post a Comment